Umuhimu wa kimkakati kwa maendeleo ya Burundi

                                                  TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali ya Burundi, kupitia Wizara ya Rasilimali Madini, Nishati, Viwanda, Biashara na Utalii, imeimarisha ushirikiano wa viwanda na Kundi la Makampuni ya Kiluwa kufuatia ziara rasmi ya kikazi iliyofanyika Dar es Salaam, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuanzia tarehe 5 hadi 10 Juni 2026.

Mheshimiwa Waziri wa Rasilimali Madini, Nishati, Viwanda, Biashara na Utalii, Dkt. Hassan Kibeya, akiambatana na Balozi wa Jamhuri ya Burundi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Léontine Nzeyimana, Mkurugenzi Mkuu wa SONALEC, Bwana Jean Baptiste Ntakirutimana, pamoja na Mkuu wa Kitivo cha Uchumi na Uongozi Chuo kikuu cha Burundi, Dkt. Suwadu Bugoma, miongoni mwa wengine, amehitimisha kwa mafanikio ziara rasmi ya kikazi katika Kundi la Makampuni ya Kiluwa nchini Tanzania. Ziara hii ililenga kuimarisha ushirikiano wa viwanda na kuendeleza uwezekano wa ubia wa kimkakati wa uwekezaji.

Ziara hii iliyoongozwa na Mheshimiwa Waziri wa Rasilimali Madini, Nishati, Viwanda, Biashara na Utalii ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali ya Burundi wa kuharakisha ujenzi wa viwanda, kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje, kuongeza thamani ya bidhaa, na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda, kulingana na dira za maendeleo za Vision 2040 na Vision 2060 za nchi hiyo.

Kuimarisha ushirikiano wa viwanda na ubia wa uwekezaji

Katika ziara hii, ujumbe wa Burundi ulifanya mazungumzo ya ngazi ya juu na majadiliano ya kiufundi na Kundi la Makampuni ya Kiluwa, mojawapo ya makundi makubwa ya viwanda nchini Tanzania yenye uwekezaji katika sekta za utengenezaji, nishati jadidifu, huduma za kusaidia uchimbaji madini, uhandisi wa usafiri, maendeleo ya viwanda vya kilimo, na bidhaa za afya.

Ujumbe huu ulipata fursa ya kutathmini uwezo wa viwanda wa Kiluwa Group na kuchunguza maeneo ya ushirikiano, ikiwa ni pamoja na usindikaji na uongezaji thamani wa madini, maendeleo ya nishati jadidifu, viwanda vya utengenezaji, miundombinu ya usafiri, uzalishaji wa mbolea, na mnyororo wa thamani wa kilimo.

Eneo kuu za ushirikiano zilizobainishwa

Majadiliano yalijikita katika nguzo sita kuu za kimkakati ambazo ni: sekta ya madini na kuongeza thamani, maendeleo ya nishati jadidifu, viwanda na maeneo ya viwanda (industrial parks), miundombinu ya reli na usafiri, maendeleo ya viwanda vya kilimo, pamoja na kukuza uwekezaji na ubia wa kimkakati.

Pande zote mbili zilibaini fursa muhimu za ushirikiano katika usindikaji wa madini, maendeleo ya nishati ya jua, miundombinu ya viwanda, uhandisi wa reli, uendelezaji wa kilimo kwa kutumia teknolojia za kisasa, na uzalishaji wa dawa, miongoni mwa maeneo mengine.

Kuelekea mfumo rasmi wa ubia

Ziara hii ilihitimishwa kwa kuandaliwa kwa mfumo wa awali wa ushirikiano pamoja na ramani ya utekelezaji itakayooongoza ushirikiano wa baadaye kati ya pande hizo mbili. Makubaliano ya Hati ya Maelewano (MoU) yanatarajiwa kuanzishwa ili kurasimisha ushirikiano katika sekta muhimu zikiwemo miundombinu, madini, nishati, kilimo, viwanda, dawa, na urahisishaji wa biashara.

Aidha, inatarajiwa kuanzishwa kwa kikundi kazi cha pamoja cha kiufundi kitakachofuatilia utekelezaji, kusimamia tafiti za upembuzi yakinifu, na kuhakikisha ufuatiliaji wa miradi ya kipaumbele.

Umuhimu wa kimkakati kwa maendeleo ya Burundi

Ziara hii inalingana kikamilifu na vipaumbele vya kitaifa vya Burundi vya kuendeleza mabadiliko ya viwanda, ajira, maendeleo ya ujuzi, na mseto wa uchumi.

Ziara hii imewezesha kupata maarifa muhimu kuhusu mifumo jumuishi ya maendeleo ya viwanda inayoweza kusaidia uzalishaji wa ndani, kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje, na kuongeza thamani ya bidhaa katika sekta muhimu.

Msisitizo maalum umewekwa kwenye usalama wa nishati, uongezaji thamani wa rasilimali madini, uboreshaji wa miundombinu ya usafiri, na maendeleo ya viwanda vya kilimo kama vichocheo muhimu vya ukuaji endelevu wa uchumi.

Dhamira ya ushirikiano wa muda mrefu

Pande zote mbili zimeahidi kuimarisha ushirikiano wa nchi mbili na kukuza fursa za uwekezaji zenye manufaa kwa pande zote. Ushirikiano huu unatarajiwa kuchangia uhamishaji wa teknolojia, ujenzi wa uwezo, maendeleo ya sekta binafsi, na ushirikiano wa kiuchumi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hatua zinazofuata

Baada ya ziara hii, Wizara ya Rasilimali Madini, Nishati, Viwanda, Biashara na Utalii pamoja na Kiluwa Group wataendelea na yafuatayo:

  • Kukamilisha Hati ya Maelewano (MoU);
  • Kuanzisha kikundi kazi cha pamoja cha kiufundi;
  • Kuandaa ramani ya utekelezaji ya ushirikiano;
  • Kufanya tafiti za upembuzi yakinifu kwa miradi iliyotambuliwa;
  • Kuandaa ziara nyingine za kiufundi za ufuatiliaji.

Hitimisho

Ziara hii rasmi ya kikazi ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na viwanda kati ya Burundi na Tanzania. Inaweka msingi imara wa ubia wa kimkakati wa muda mrefu unaolenga kuharakisha maendeleo ya viwanda, kukuza uwekezaji, na kusaidia mabadiliko endelevu ya kiuchumi ya Burundi.

Imetolewa na:

Wizara ya Rasilimali Madini, Nishati, Viwanda, Biashara na Utalii

Jamhuri ya Burundi

Bujumbura, tarehe 11/06/2026

Idara ya Mawasiliano na Nyaraka